Kila mwaka, zaidi ya wanawake milioni 2.3 hugunduliwa na saratani ya matiti, na karibu 700,000 hufa kutokana na ugonjwa huo, ambao huathiri vibaya wanawake wanaoishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati.
Maafisa wa WHO wanasema wanawake wanaoishi katika nchi maskini wana uwezekano mdogo sana wa kunusurika na saratani ya matiti kuliko wanawake katika nchi tajiri zaidi. Kupona saratani ya matiti ni asilimia 50 au chini katika nchi nyingi za kipato cha chini na cha kati, na zaidi ya asilimia 90 kwa wale wanaoweza kupata huduma bora katika nchi zenye kipato cha juu, anasema Bente Mikkelsen, mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza katika shirika la WHO.
Anasema uwezekano huo umekuwa mgumu dhidi ya wanawake wanaoishi katika nchi maskini, akibainisha kuwa wengi lazima wauze mali zao ili kulipia matibabu wanayohitaji.