DRC: Kundi la waasi la M23 lashtumiwa kushambulia walinda amani wa Umoja wa mataifa

Jeshi la Umoja wa Mataifa la Monusco nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wameanza ushirikiano mpya na jeshi tiifu la serikali ya nchi hiyo katika operesheni dhidi ya waasi wa M23 wilayani Rutshuru, Kivu kaskazini. Picha iliyopigwa na Austere Malivika

Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa mataifa Jumapili amelishtumu kundi la M23 linaloendesha harakati zake nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kushambulia walinda amani wa tume ya Umoja wa mataifa katika eneo la mashariki mwa nchi lenye machafuko.

Taarifa hiyo ya Bintou Keita, mwakilishi wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa inajiri baada ya jeshi la DRC kuanzisha mashambulizi dhidi ya kundi la M23 siku ya Alhamisi.

Taarifa ya Keita imelaani shambulio la kundi hilo dhidi ya wanajeshi wa serikali na kikosi cha walinda amani wa MONUSCO.

“Waasi wa M23 walilenga kwa makusudi walinda amani wa Monusco ambao walijibu kwa risasi, kulingana na mamlaka yao,” Keita amesema.

Jeshi la DRC na wanajeshi wa Monusco walianzisha operesheni ya pamoja dhidi ya waasi wa M23, taarifa ya Keita imeongeza.

Wakazi wa mji wa Goma wamesema Monusco ilitumia helikopta katika operesheni hiyo dhidi ya waasi wa M23.

Taarifa ya M23 imesema wapiganaji wao walilazimisha wanajeshi wa serikali kurudi nyuma na walikimbilia kwenye kambi ya Monusco, na hivyo kuwalazimu walinda amani wa Umoja wa mataifa kuingilia kati.