Muigizaji maarufu, Debbie Reynolds ameaga dunia, siku moja baada ya kifo cha mwanawe, Carrie Fisher ambaye naye alikuwa muigizaji maarufu duniani.
Lakini saa chache kabla ya kutangazwa kifo chake, idara ya zimamoto ya Los Angeles ilithibisha kwamba mwanamke mtu mzima alipelekwa katika kituo cha afya cha Cedars-Sinai Los Angeles, vimesema baadhi ya vyanzo vya habari hapa Marekani.
Debbie Reynolds, 84, alikuwa ni msanii mashuhuri wa muda mrefu, aliyetambulika katika wimbo wa kifahari wa Singin’ in the Rain- nyota wa televisheni- kwenye kipindi cha Debbie Reynolds- na supasta huko Broadway na Las Vegas.
Jina lake tayari limependekezwa kwa ajili ya tuzo mbili maarufu kuliko zote za Academy Award, zinazojulikana kama Emmy na Golden Globe.
Mwaka 2015, alishinda tuzo nyingine maarufu ya Jean Hersholt Humanitarian Award kutoka chuo cha sanaa za picha na sayansi.
Moja ya sifa za msanii huyu ni uana harakati wake katika kuhamasisha watu kufahamu afya ya akili akishirikiana na mtoto wake ambaye alikuwa na matatizo ya akili.
Mama na mtoto walikuwa ni wenye kushibana na kupendana kupita kiasi. Hilo limeelezewa katika kitabu chake Fisher kinachoitwa “Postcards from the Edge,” ambacho baadae kilitengenezwa kuwa filamu.
Kwa upande wake Fisher alitutoka Jumanne baada ya kupata mshtuko wa moyo siku ya Ijumaa akiwa kwenye ndege akitoka London kwenda Los Angeles.