Kiwanda cha kusafishia mafuta cha Dangote cha Nigeria kitakacho zalisha mapipa 650,000 ya mafuta kwa siku kinafanyiwa majaribio ya uzalishaji wa petroli, huku kikitarajiwa kufanyakazi kikamilifu kufikia katikati ya Septemba, kwa mujibu wa dokezo la kampuni ya kufuatilia IIR Energy.
Kiwanda cha kusafishia mafuta cha Dangote chenye thamani ya dola bilioni 20, kilichojengwa na tajiri mkubwa zaidi barani Afrika, Aliko Dangote, katika viunga vya jiji la Lagos, kilianza kufanya kazi Januari baada ya kuchelewa kwa miaka mingi.
Dangote, ambaye hadi sasa anazalisha tu dizeli na aina ya mafuta mengine, awali alisema kuwa uwasilishaji wa petroli kutoka kwenye kiwanda cha kusafisha mafuta utaanza Julai.
Kabla ya hapo kiwanda hicho kilikuwa na lengo la kuanza kutengeneza mafuta ya mashine ifikapo mwezi Mei.