Cyril Ramaphosa katika mtihani mkubwa kwenye uchaguzi ujao Afrika Kusini

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akizungumza katika mkutano wa kampeni huko Chatsworth

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ambaye ameweka heshima yake katika kusafisha sura ya chama tawala cha African National Congress, atakiongoza chama hicho kuelekea mtihani wake mkubwa zaidi wa enzi ya  kidemokrasia wakati Waafrika Kusini watakapopiga kura siku ya Jumatano.

Ramaphosa, ambaye alisaidia kuanzishwa kwa chama kikubwa zaidi cha madini nchini humo na baadaye kuwa mmoja wa wafanyabiashara wake tajiri sana, alichukua wadhifa wa urais mwaka 2018 na kunusurika katika kashfa ya utovu wa nidhamu na kuchaguliwa tena kushika usukani wa ANC mwaka 2022.

Amepambana kuinua ukuaji wa uchumi, kushughulikia uhaba mkubwa wa ajira huku theluthi moja ya Waafrika Kusini wakiwa hawana ajira, au kumaliza kukatika kwa umeme jambo ambalo wapiga kura wanatarajiwa kuiadhibu ANC katika sanduku la kura kesho Mei 29.

Iwapo chama hicho kitapoteza wingi wake kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30, kama kura za maoni zinavyotabiri, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema Ramaphosa mwenye umri wa miaka 71 huenda asipate muhula wa pili.