Comey ambaye alifukuzwa kazi na Trump hivi karibuni, amesema akiwa Jengo la Bunge la Marekani Alhamisi kuwa maafisa wa ikulu ya White House walieneza uzushi uliokuwa wazi ili kuficha sababu zilizopelekea yeye kufukuzwa.
“Hakuna shaka kuwa nilifukuzwa kwa sababu ya kuichunguza Russia,” Comey aliwaambia Maseneta, akielezea kuongezeka kwa uchunguzi unaofanywa kubaini jinsi Russia ilivyoingilia kati uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka jana.
Kuingilia kati huko kwa Russia kumeelezwa na vyombo vya usalama ilikuwa ni juhudi ya Kremlin kumsaidia Trump kushinda uchaguzi dhidi ya hasimu wake Mdemokrat, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Hillary Clinton.
Juhudi za Rais “kubadilisha jinsi uchunguzi dhidi ya Russia unavyofanyika, hilo ni jambo kubwa,” Comey amesema.
Ushuhuda wa Comey mbele ya Kamati ya Usalama ya Baraza la Seneti ilikuwa ni fursa yake ya kwanza kuzungumza kwa umma kuhusu mikutano yake na mazungumzo aliofanya na Trump katika miezi kadhaa kabla ya kufukuzwa kazi.
Mkuu wa zamani huyo wa shirika la kusimamia utekelezaji wa sheri alihojiwa mara kadhaa na Warepublikan na Wademokrat katika muda mmoja wakipeana zamu kumsaili Comey kwa takriban masaa matatu; na kilikuwa na mvuto kwa wengi na kutangazwa mubashara na vituo vyote vikubwa vya televisheni na kutangazwa dunia nzima.