Clinton na Trump kuchuana kwenye mdahalo mjini New York jumatatu usiku

Bi. Hillary Clinton and Donald Trump watachuana kwenye mdahalo mjini New York jumatatu usiku.

Mdemokrat Hillary Clinton na mrepublikan Donald Trump watapambana katika mdahalo wao wa kwanza kati ya mitatu katika chuo kikuu cha Hempstead New York Jumatatu usiku saa za Marekani.

Hili linatarajiwa kuwa moja ya tukio litakalotazamwa kwa kiasi kikubwa kuliko mengine ya urais hapa Marekani na inaweza kuwa na athari katika matokeo ya uchaguzi wa rais.

Mdahalo huu utakuwa ni tukio muhumu kwa Donald Trump ambaye hivi karibuni amemkaribia mpinzani wake Hillary Clinton kwenye uchunguzi wa maoni.

Clinton ataingia kwenye mdahalo huo kuwapa uhakika waunga mkono wake na kusukuma ujumbe wake wa kutaka kujenga uchumi wa kujumuisha watu wote.

Ukumbi wa mdahalo uko tayari kwa wakati muhimu katika uchaguzi wa rais wa Marekani 2016 ambapo wagombea hao watapambana kwa dakika 90.

Wagombea hao wawili wako kwenye mchuano mkali, huku ukusanyaji wa maoni kitaifa ukionyesha Clinton akiongoza kwa asilimia ndogo.

Kwa mamilioni ya wamarekani watakaoangalia televisheni itakuwa ni mara ya kwanza kuwaona wagombea hao wakiwa jukwaani uso kwa uso wakielezea misimamo yao kuhusu masuala makuu yanayoikabili nchi, na kutathmini majibu kwa kauli ya kila mmoja wao aliyoitoa, na kufikiria ikiwa mmoja wao atakuwa rais wa 45 wa nchi hii kwa kipindi cha miaka mine ijayo.