Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton amesema Washington itachukua msimamo wa kusubiri na kutizama kutokana na kujihusisha kwa wanaharakati wa Kislamu wa Misri katika mazungumzo na serikali juu ya ghasia za kisiasa nchini humo.
Katika mahojiano na radio ya Marekani NPR, Jumapili, Bi.Clinton amesema uamuzi wa Muslim Brotherhood kujiunga na kuzungumza na serikali inaonyesha kwamba inajihusisha na aina ya majadiliano ambayo Washington ilipendekeza na kuhimiza. Alikuwa akizungumza wakati wa ziara yake huko Ujerumani.
Clinton amesema Marekani imeshaeleza bayana kile inachokitegemea kutokana na mazunguzo ya Cairo, yani mpiyto wa mpangilio katika kukabidhana madaraka kutoka kwa rais wa muda mrefu wa Misri Hosni Mubarak, na kupelekea uchaguzi wa huru na haki . Amesema hicho ndicho raia wa Misri wanachotaka.
Katika mahojiano tofauti kwnye kituo cha televisheni cha NBC, kipindi cha Meet The Press, mwenyekiti wa kamati ya masuala ya kigeni katika baraza la Seneta la Marekani John Kerry, amepongeza mazungumzo kati ya serikali na upinzani akieleza kuwa ni jambo la kipekee na kumhimiza Rais Mubark kuanza utaratibu wa mpito kuelekea utawala mpya.
Hata hivyo kiongozi mashuhuri wa upinzani Misri Mohamed ElBaradei amekosoa mazungumzo ya Jumapili huko Cairo akiyaeleza kwamba hayako wazi na kwamba hakualikwa kuhudhuria mazungumzo hayo. Akizungumza na kipindi hicho cha Meet The Press ElBaradei alisema kumebaki mwanya mkubwa sana wa kuaminiana kati ya serikali na waandamanaqji.