Chombo 'Insight' cha Marekani chatua salama Mars

Chombo cha anga za juu, Insight, kilichotua kwenye sayari ya Mars.

Safari ya anga za juu ya chombo cha kipekee, kilichopewa jina Insight ilikamilika Jumatatu, pale chombo hicho kisicho na rubani na kinachotumia teknolojia ya kisasa kabisa, kilipotua kwenye sayari ya Mars.  Safari hiyo imekuwa ikiangaziwa kwa karibu mno tangu chombo hicho kuondoka ardhini.

Ilikuwa ni furaha kubwa kwa wahandisi na wafanyakazi wa Shirika la Marekani la kuratibu safari za anga za juu, NASA, pale ilipotangazwa kwamba Insight ilitua salama salimini kwenye Mars, maarufu kama sayari nyekundu.

Baada ya kusafiri kwa maili milioni mia tatu na kwa muda wa takriban miezi saba, hatimaye chombo hicho kilipunguza mwendo wake na kutua taratibu, huku wafanyakazi na wahandisi wa NASA wakifuatikia kwa karibu kutoka maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kituo cha kimataifa cha anga za juu.

Hapa duniani, mamilioni ya Wamarekani walitazama chombo hicho kikitua kupitia picha zilizorushwa moja kwa moja na Satetellite za kituo cha televisheni cha NASA, na kuonyeshwa katika maeneo mbalimbali nchini kote.

Wafanyakazi wa NASA washerehekea baada tya kupata uthibitisho kwamba Insight imetua salama kwenye sayari ya Mars.

Maelfu ya watu walikusanyika katika mtaa wa Times Square mjini New York, Marekani kushuhudia tukio hilo la kihistoria.

Mkurugenzi wa NASA, Jim Bridenstine, alisema kutua kwa Insight , ni tukio ambalo limewapa montisha sana wafanyakazi wa shirika hilo, hususan kwa sababu wengi walikuwa na wasiwasi kwamba huenda safari hiyo isifaulu, kutokana na changamoto zilizoshuhudiwa wakati wa misheni zingine kama hizo hapo awali.

Muda mfupi baada ya tangazo kwamba chombo hicho kilikuwa kimetua, Makamu wa rais wa Marekani, Mike Pence, alimpigia simu mkurugenzi huyo, na kumpongeza pamoja na timu yake.

Maaafisa wa NASA wamesema kwamba chombo hicho kina majukumu maalum, ikiwa ni pamoja na kupenya na kuingia futi kadhaa ndani ya mchanga wa Mars ili kupata tathmini ya iwapo viwango vya joto vinaweza kuruhusu binadamu kuishi kwenye sayari hiyo.

Aidha roboti hiyo, ambayo inatumia nguvu za jua kama nishati yake, inatarajiwa kuchora ramani itakayotumiwa katika siku za usoni.

Mchoro wa kompyuta ukionyesha hali ilivyokuwa wakati chombo 'Insight' kilipotua kwenye sayari ya Mars.

NASA imetuma vifaa mara saba kwenye sayari hiyo katika kipindi cha miongo minne. Moja ya safari hizo hata hivyo, haikufua dafu.

Chombo hicho kinatarajiwa kukaa kwenye sayari ya Mars kwa takriban miaka miwili kikifanya utafiti kabla ya kurejea duniani.

Licha ya kufaulu kwa safari hiyo na zingine za awali, NASA inakadiria kwamba binadamu hatatua kwenye Sayari hiyo kabla ya mwaka wa 2030.