Chirac wa Ufaransa akutwa na makosa ya rushwa

Rais wa zamani wa Ufaransa, Jacgues Chirac (katikati) akiwa ndani ya gari mjini Paris, Ufaransa

Mahakama moja mjini Paris imemkuta na makosa ya rushwa Jacques Chirac wakati akiwa madarakani

Rais wa zamani wa Ufaransa Jacques Chirac amekutwa na hatia katika mashtaka ya rushwa nchini mwake.

Jaji mmoja nchini humo alimkuta bwana Chirac na makosa ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika kesi iliyosikilizwa Alhamis, lakini aliahirisha hukumu yake ya miaka miwili katika kesi hiyo.

Alikuwa Rais wa kwanza wa zamani nchini Ufaransa kufikishwa mahakamani kwa mashtaka hayo kwa zaidi ya miaka 50.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 79, ambaye hakuwepo wakati kesi ikisomwa kwa sababu ya matatizo ya afya, alikutwa na makosa ya matumizi mabaya ya fedha za umma na kutumia vibaya madaraka yake wakati alipokuwa meya wa Paris, kati ya mwaka 1977 hadi 1995.

Bwana Chirac amekuwa akirudia kukana kuwa hajafanya kosa lolote. Watu tisa wengine pia wamehusishwa katika kesi hiyo.

Bwana Chirac alishutumiwa kuwalipa wanachama wake wa chama cha Rally for the Repuplican, kwa kutumia fedha za manispaa ambapo alibuni ajira zisizo na maana ndani ya manispaa kwa watu hao.

Alikuwa anakabiliwa na kifungo cha juu kisichopungua miaka 10 na kutakiwa kulipa faini ya dola 160,000.