China yazidisha doria karibu na Taiwan

China inazidisha doria katika katika pwani ya visiwa vya Kinmen vya Taiwan, siku chache baada ya wavuvi wake wawili kufa maji walipokuwa wakifukuzwa na walinzi wa pwani wa Taiwan, ambao waliishutumu mashua hiyo kwa kuingia eneo hilo bila ya ruhusa.

Walinzi wa pwani ya China, wa kitengo cha Fujian, watafuatilia mara kwa mara pwani ya kusini ya mji wa Xiamen, kilomita chache kutoka Kinmen, ili kuimarisha utekelezaji wa sheria za baharini, msemaji wa walinzi wa pwani, Gan Yu, amesema katika taarifa yake ya Jumapili.

Wavuvi kutoka Taiwan, na China, husafiri mara kwa mara sehemu hiyo ya maji ambayo imeshuhudia kuongezeka kwa mvutano baada ya idadi ya meli za China, zinazo chimba mchanga na boti za uvuvi zimeongezeka haswa katika eneo hilo.

Wakaazi wa Kinmen, wamelalamikia kelele na uchafuzi kutoka kwa meli hizo, pamoja na hasara ya maisha yao katika uvuvi.