China Jumanne imetetea uamuzi wake kuiruhusu Umoja wa Mataifa kumtangaza kiongozi wa wanamgambo anayeipinga India kuwa ni gaidi wa kidunia, ikisema hatua hiyo itaimarisha ushirikiano wa kimataifa wa kukabiliana na ugaidi.
Abdul Rehman Makki, mwenye umri wa miaka 68 ambaye kwa sasa anatumikia kifungo nchini Pakistan, kwa mashitaka ya ugaidi, aliongezwa katika orodha ya vikwazo na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Jumatatu.
India na Marekani kwa pamoja zilipendekeza kutajwa kwake mwezi Juni mwaka jana, lakini China, mshirika wa karibu wa Pakistan, iliweka kikwazo ilichosema cha kiufundi cha kusubiri mapendekezo ambacho imekiondoa Jumatatu.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Wang Wenbin, aliuambia mkutano wa kawaida na wanahabari kwamba ugaidi ni adui wa kila mmoja.