Baada ya kushinikizwa na Kiongozi wa walio wengi katika baraza la Seneti la Marekani Chuck Schumer, Beijing imelaani mashambulizi yaliyofanywa na Hamas nchini Israel lakini ilifanya hivyo bila kuitaja Hamas.
Katika taarifa ya hivi karibuni kutoka kwa Wizara yake ya Mambo ya Nje, China imelaani "ghasia zote na mashambulizi dhidi ya raia" na kusema "kazi ya dharura zaidi sasa ni kufikia usitishaji vita na kurejesha amani."
Kauli hiyo iliyotolewa Jumatatu ilikuja baada ya Schumer, mdemokrat kuelezea kusikitishwa kwake na kiongozi wa China Xi Jinping juu ya taarifa ya awali ya China ambayo ilitaka tu kusitisha mapigano.
"Nilizungumza na Rais Xi kuhusu ukatili unaoendelea kufanywa dhidi ya Israel na haja ya jumuiya ya kimataifa kusimama pamoja dhidi ya ugaidi na watu wa Israel na nilimwomba Rais Xi kwamba waziri wa mambo ya nje wa China aimarishe kauli yao; walifanya hivyo," Schumer. alisema katika taarifa yake Jumatatu.