Ndege ya mizigo iliyokuwa imebeba tani 45 za mbegu za Pine Jumapili imeondoka kwenye uwanja wa ndege wa Kabul kuelekea kwenye masoko ya China, ikiashiria ukurasa mpya wa kibiashara kati ya mataifa hayo tangu Taliban kukamata serikali mwezi Agosti.
Msemaji wa serikali ya Taliban Bilal Karimi ameiambia VOA kwamba wanatumai shughuli za kibiashara zitaendelea kuimarika kati ya taifa lake na China.
Amesema kwamba hatua hiyo ni kufuatia mashauriano ya hivi karibuni kati ya Kabul na Beijing, akiongeza kwamba wanapiga hatua kuelekea kwenye ushirikiano zaidi katika siku zijazo. China ndilo soko kubwa zaidi la mbegu za Pine kutoka Afghanistan.
Wakati biashara hiyo ilipofunguliwa awali mwaka 2018, wataalamu walikisia kwamba Afghanistan ingepeleka tani 23,000 za bidhaa hiyo kila mwaka nchini China, wakati ikijipatia takriban dola milioni 800.