China na Australia zinaweka mikakati ya kuimarisha diplomasia

Wafanyakazi katika bandari ya Yingkou, kaskazini mashariki mwa China July 24 2019

Waziri wa mambo ya nje wa Australia Penny Wong amefanya mazungumzo na mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa China mjini Jakarta, na kusema mazungumzo hayo kuwa ya kweli.

Wong amefanya mazungumzo na mkuu wa maswala ya mambo ya nje wa chama tawala nchini China cha kikomunisti Wang Yi, pembeni mwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama wa ASEAN, unaoendelea Jakarta, Indonesia.

Australia imetoa wito kwa China kuendelea kuondoa vizuizi kwa bidhaa kutoka Australia, vilivyowekwa wakati uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili ulipokuwa mbaya.

China imeanza kuruhusu uagizaji wa makaa ya mawe, mbao, mvinyo na Kamba wa baharini, kutoka Australia lakini kiwango cha ushuru kinachotozwa kwenye bidhaa hizo kiko juu.

Wong vile vile ametaka swala la raia wa Australia wanaozuiliwa Beijing kuhusiana na mashtaka ya kiusalama, kuangaziwa.