China na Angola zaahidi kuboresha ushirikiano wa kiuchumi

Rais wa China Xi Jinping (katikati) akiwa katika mkutano wa BRICS mwaka 2023 huko Johannesburg Agosti 24, 2023. Picha na ALET PRETORIUS / POOL / AFP

Rais Xi Jinping wa China na Rais wa Angola Joao Lourenco Ijumaa walitangaza kuboresha uhusiano wa pande mbili na ushirikiano wa kimkakati.

Xi alimueleza Lourenco kwamba China iko tayari kufanya kazi na mzalishaji mafuta wa Afrika katika miradi muhimu ya miundombinu na itaunga mkono makampuni ya China ambayo yanawekeza katika sekta za kilimo na viwanda huko Angola.

Uamuzi huo ulitolewa wakati wa mazungumzo kati ya Xi na Joao Lourenco, ambaye yuko katika ziara ya kiserikali nchini China pia kufuatia tangazo la Angola la mwezi Desemba kuwa itaondoka katika Jumuiya ya Nchi Zinazouza Mafuta -- OPEC na kuingia makubaliano na China kuhusu ushirikiano.

Xi amesema, kutokana na mabadiliko na utaratibu duniani, China na Angola zinapaswa kuendeleza mafanikio, kusaidiana na kushirikiana ili kuboresha maendeleo, na kuinua ushirikiano wao.

Lourenco anafanya ziara ya kiserikali nchini China kuanzia Machi 14 hadi 17 kwa mwaliko wa Xi.