China imeonya mataifa ya kundi la G7 yenye utajiri kiviwanda dhidi ya kufanya mazungumzo yanayoweza kuharibu hali zaidi kwenye mzozo wa South China Sea.
Mizozo ya bahari ni mojawapo ya maswala makuu yanayotarajiwa kujadiliwa kwenye mkutano wa mataifa hayo wiki hii mjini Tokyo.
Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa G7, Rais Barack Obama wa Marekani amesema leo kuwa viongozi wa kundi hilo watajadili kuhusu South China Sea miongoni mwa maswala mengine ya kimataifa.
Mwezi uliopita, mawaziri wa kigeni kutoka kundi hilo walitoa taarifa ya pamoja kuhusu usalama wa bahari wakati wa kumaliza mkutano wao wakielezea wasiwasi kuhusu East China Sea na South China Sea. Ingawa taarifa hiyo haikutaja China, Beijing imelaumu kundi hilo kwa kuegemea upande mmoja.