China imemruhusu balozi wa Canada kukutana na raia wa pili wa Canada aliyetiwa ndani kwa sababu ambazo bado haziko bayana ilieleza wizara ya mambo ya nje huko Ottawa.
Balozi John McCallum alizungumza na mtendaji mkuu wa biashara wa Canada Michael Spavor siku ya Jumapili ikiwa ni siku mbili baada ya kukutana na raia mwingine wa Canada aliyekamatwa mwanadiplomasia wa zamani Michael Kovrig.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ilieleza Jumapili kuwa balozi McCullum ataendelea kutoa huduma za kibalozi kwa Spavor na ataomba kupata fursa zaidi ya kuonana nae.
China iliwakamata wanaume wote hao wawili baada ya polisi wa Canada kumkamata mtendaji mkuu wa kampuni ya teknolojia ya China, Meng Wanzhou mwanzoni mwa mwezi huu mjini Vancouver kufuatia waranti ya Marekani. Meng yupo nje kwa dhamana anasubiri uwezekano wa kusafirishwa kwenda Marekani kujibu mashtaka ya kukiuka vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.