Chanjo ya majaribio dhidi ya ebola kuanza kutolewa Uganda

Waziri wa afya wa Uganda Jane Ruth Aceng akipokea masanduku yenye chanjo ya majaribio dhidi ya ebola, Entebbe, Uganda Dec 8, 2022.

Serikali ya Uganda imesema kwamba imepokea zaidi ya dozi 5,000 za chanjo ya majaribio dhidi ya virusi vya Ebola aina ya Sudan ambavyo vimesababisha vifo vya watu 50 nchini humo.

Waziri wa afya Jane Ruth Aceng, amewaambia waandishi wa habari kwamba mashauriano ya kitaalamu duniani yatafanyika Januari 12 ili kuamua siku ambayo utoaji wa chanjo hiyo ya majaribio utaanza.

Tangazo la serikali ya Uganda limetolewa siku moja kabla ya shirika la afya duniani WHO kutangaza kwamba Uganda haina maambukizi ya virusi vya ebola baada ya maambukizi mapya kutoripotiwa ndani ya siku 42.

Watu 142 wameambukizwa virusi vya Ebola, na watu 56 wamefariki tangu mwezi Septemba mlipuko wa virusi hivyo ulipotangazwa.

Aina ya Ebola ya Sudan isiyokuwa na chanjo, ni tofauti na aina ya Zaire ambayo imekuwa ikitoka Congo katika miaka ya hivi karibuni.

Mlipuko wa Ebola aina ya Sudan, ambao umetokea nchini Uganda ni wa kwanza baada ya miongo kadhaa na aina tatu ya chanjo ya majaribio imetolewa na taasisi ya chanjo ya Sabin ya nchini Marekani, chuo kikuu cha Oxford na Merck.

Waziri wa afya wa Uganda amesema kwamba chanjo itatolewa kwa hiari na kwamba haitatolewa kwa sababu nyingine isipokuwa ya majaribio.

Virusi vya Ebola husambaa kutoka kwa mgonjwa hadi kwa mtu mwingine kupitia maji maji ya mwili kama jasho.

Shirika la afya duniani limesema kwamba asilimia 40 ya wagonjwa wa ebola aina ya Sudan, wanafariki.