Chanjo ya Covid-19 yaanza kutolewa Uingereza

Bi Margaret Keenan, 90, mtu wa kwanza kupewa chanjo ya Corona ya Pfizer/BioNtech.

Margaret Keenan, bibi mwenye umri wa miaka 90 kutoka Ireland Kaskazini leo amekuwa mtu wa kwanza duniani kupewa chanjo dhidi ya virusi vya corona ya kampuni ya Pfizer, wakati Uingereza imeanza kutoa chanjo kwa raia wake.

Keenan amepata chanjo hiyo ya kampuni ya Pfizer-BioNTech asubuhi majira ya uingereza, wiki moja kabla ya kutimiza miaka 91.

Uingera imekuwa nchi ya kwanza ya magharibi kuidhinisha chanjo kwa raia wake na imepongezwa kwa kuchukua hatua hiyo katika juhudi za kutokomeza virusi vya Corona.

“Nahisi ni bahati kubwa kuwa mtu wa kwanza kupewa chanjo dhidi ya covid 19,” alisema Keenan.

Uingereza ni moja ya nchi za magharibi zilizoathirika mno kutokana na janga la Covid 19, ikiripoti vifo elfu 61 kutokana na ugonjwa huo.

-Imetayarishwa na Patrick Nduwimana, VOA, Washington DC