Chama tawala nchini Zimbabwe chapata wingi wa viti bungeni baada ya kushinda uchaguzi mdogo

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa

Chama tawala nchini Zimbabwe cha ZANU-PF sasa kinaongoza kwa theluthi mbili ndani ya bunge na kinaweza kufanya marekebisho ya katiba na kuimarisha mamlaka ya Rais Emmerson Mnangangwa, baada ya matokeo ya uchaguzi mdogo kutangazwa Jumapili.

Chama hicho kimepata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliofanyika Jumamosi katika maeneo bunge sita baada ya utaratibu wa kipekee wa kisiasa uliokosolewa na upinzani kuwa udanganyifu ambao ulisababisha wabunge sita wa upinzani kuondolewa.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Zimbabwe Rodney Kiwa ameiambia AFP kwamba “Uchaguzi ulikwenda vizuri. ZANU-PF imeshinda katika maeneo bunge yote sita. Ninathibitisha ushindi huo.”

Hii ni mara ya pili kwa Zimbabwe kufanya uchaguzi mdogo wa bunge tangu kuzuka kwa mzozo wa kisiasa ambao umedhoofisha upinzani na sasa unaweza kuimarisha mamlaka ya Mnangagwa mwenye umri wa miaka 81.

Wachambuzi na wanaharakati wa upinzani wanaonya kwamba ZANU-PF sasa inaweza kuwa na wingi wa viti 190 bungeni kati ya 280, na viti viwili vikiwa wazi, kuna uwezekano wa kuondoa ukomo wa mihula miwili ya urais na kumruhusu Mnangangwa kugombea tena.