Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe cha Citizens Coalition for Change (CCC) Jumanne kimeomba uitishwe uchaguzi mpya baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliopita na kuutaja kuwa wenye udanganyifu.
Naibu msemaji wa CCC Gift Siziba ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba chama chao kimetoa wito kwa Umoja wa Afrika na Jumuia ya Madola ya Kusini mwa Afrika SADC kusuluhisha kurejea kwa utawala halali nchini Zimbabwe.
Tume ya uchaguzi siku ya Jumamosi ilimtangaza rais aliye madarakani Emmerson Mnangagwa wa chama tawala cha ZANU-PF mshindi wa uchaguzi wa rais wa wiki iliyopita, lakini wachambuzi wamehoji sana uaminifu wa matokeo.