IMF imesema wiki hii wanasiasa wa ngazi ya juu chini ya rais wa zamani Edgar Lungu, walikiuka sheria ili kupata kandarasi za serikali zenye faida kubwa.
Rais wa sasa Hakainde Hichilema, aliahidi kukabiliana na ufisadi na kupata dola bilioni 1.3 za kusaidia katika kulipa madeni ya IMF baada ya Zambia kutolipa mikopo.
Ujumbe wa IMF ulifanya utafiti mwaka jana ukiangazia udhaifu wa utawala na rushwa nchini Zambia kwa ombi la serekali.
Tathmini hiyo ilibaini udhaifu mkubwa katika kazi zote za serikali, hasa usimamizi wa fedha za umma na usimamizi wa kandarasi za miradi mikubwa ya miundombinu.
Ilisema gharama za miradi ya hadhi ya juu ziliongezwa kwa kiasi cha asilimia 200 chini ya utawala wa Rais Edgar Lungu, huku pesa za ziada zikiingia kwenye mifuko ya wafuasi wa Lungu wenye uhusiano naye mzuri.
Maafisa kadhaa wa zamani wa serikali walikamatwa kwa tuhuma za ufisadi. Hata hivyo, kamatakamata hiyo iliishia kwenye dhamana, huku washtakiwa wakikana mashtaka. Hakuna aliyekutwa na hatia.
Msemaji wa chama cha Patriotic Front, Raphael Nakachinda alikanusha madai ya IMF ya ufisadi mkubwa chini ya utawala wa rais wa zamani Edgar Lungu.
Nakachinda aliiambia VOA kuwa wakiwa serikalini, Patriotic Front iliweka mikakati ya kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika manunuzi ya umma.
Alitoa changamoto kwa serikali iliyopo madarakani kuchukua hatua za kisheria dhidi ya viongozi wake wa zamani ambao watabainika kushiriki hayo.
"Tulihakikisha tulipokuwa madarakani mikataba yote ya serikali inapitia mchakato mkali wa zabuni ya umma ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji na kuna sheria za kutosha Zambia kuruhusu wananchi kupinga, kukata rufaa au kupinga mchakato wowote wa mikataba ya serikali yenye ufisadi. Mchakato wa zabuni ni mchakato wa umma na kwa hivyo tuhuma hizo ni uzushi."
Msemaji wa rais Anthony Bwalya, aliiambia VOA kwamba ripoti ya IMF ni uthibitisho wa kile ambacho serikali ya Rais Hakainde Hichilema imefahamu kwamba rushwa ya Zambia ilishamiri zaidi wakati wa utawala wa Lungu.
"Hii ndiyo sababu rais ameweka kipaumbele cha msingi kushinda vita dhidi ya ufisadi kama sehemu ya mchakato wa kujenga uchumi. Tumeanzisha mahakama za uhalifu wa kifedha ili kuharakisha mchakato wa kuwawajibisha wahusika wa ufisadi, pia tumerekebisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma kwa uwazi bora na kurekebisha mchakato wa ununuzi wa umma.”
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, karibu theluthi mbili ya wakazi wa Zambia wanaishi chini ya dola mbili kwa siku.