Chama tawala nchini Afrika kusini cha African National Congress-ANC kinaelekea kupata ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano kulingana na matokeo ya awali yaliyoanza kutolewa Ijumaa japokuwa chama kinaelekea kupata pigo kubwa katika uchaguzi huo tangu kilipochukua madaraka miaka 25 iliyopita.
Kufikia usiku wa manane wa kuamkia Ijumaa asilimia 72 ya kura zilikwisha hesabiwa katika wilaya 22,925. Matokeo hayo yanakipatia chama cha ANC ushindi wa asilimia 57 katika uchaguzi wa bunge la taifa huku chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance-DA kikipata asilimia 22 ya kura kikifuatiwa na chama cha mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters-EFF kikiwa na asilimia 10 ya kura.
Chama kikongwe cha Nelson Mandela cha ANC hakijawahi kushinda chini ya asilimia 60 ya kura tangu kilipoingia madarakani kupitia uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1994 uliofikisha kikomo wa utawala wa watu weupe walio wachache.
Kulingana na matokeo ya mwisho kutolewa na tume ya uchaguzi ya Afrika kusini wachambuzi walibashiri ANC kitapata kati ya asilimia 55 hadi 59 ya kura. Kutojitokeza ipasavyo kwa wanachama wa ANC kupiga kura kumefanya wapinzani wa Rais Cyril Ramaphosa kujinyakulia asilimia nyingi na kutoa changamoto kwenye uongozi wake. ANC itachaguliwa kwa rekodi ya chini ya kuungwa mkono na asilimia 27 ya wapiga kura waliojiandikisha ikilinganishwa na asilimia 47 ya mwaka 1999.
Katika mtihani wa kwanza kitaifa wa Rais Ramaphosa wa-Afrika kusini walipiga kura Jumatano pia walichagua wabunge na viongozi wa mabunge ya majimbo 9 ya nchi hiyo. Wapiga kura walielezea kusikitishwa na rushwa iliyokithiri, ukosefu wa ajira na ubaguzi wa rangi ambao bado ni tatizo nchini humo.
Watu wanaonesha wapo tayari kukisamehe chama cha ANC alieleza Ronald Lamola mwanachama wa cheo cha juu wa African National Congress-ANC.