Chadema yapanga kujadili mustakbali wa demokrasia Tanzania

Freeman Mbowe

Kamati Kuu ya chama cha Demokrasia na Maendeleo nchini Tanzania imesema itakutana pamoja na wabunge na madiwani kujadili mustakabali wa demokrasia nchini na kutoa maelekezo kwa wanachama wake nini cha kufanya.

Akisoma maazimio ya Kamati Kuu iliyokutana Jumatano Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari, alisema wamekutana kwa dharura (Jumatano) na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kujadiliana kuhusu viongozi wao kuwekwa mahabusu.

Profesa Safari amesema: “Kwa hiyo tunatoa wito kwa wadau wote wa demokrasia nchini, kama vile viongozi wa dini walivyofanya na tunategemea Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania) nao watafanya hivyo kushiriki kikamilifu katika mapambano ya kudai demokrasia kwa ustawi wa wananchi wote nchini.”

"Leo tumekutana kwa dharura na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu, Alhamisi baada ya maamuzi ya mahakama kuhusu viongozi wetu kamati kuu itakutana...," aliongeza.

Juzi, viongozi hao wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe walisomewa mashtaka, wakakosa dhamana na kupelekwa Gereza la Segerea hadi leo mahakama itakapotoa uamuzi wa kupewa dhamana au laa.

Pia uongozi huo umesema kuwa bado wana imani na baadhi ya mahakimu wenye moyo wa kutenda haki.