Chadema yahoji serikali ya Tanzania inataka maombi gani juu ya matibabu ya Lissu

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeweka msimamo kwamba kitaendelea kushughulikia na kusimamia matibabu ya Mbunge Tundu Lissu ambaye alishambuliwa kwa kupigwa risasi katika eneo nyeti la makazi ya viongozi huko mjini Dodoma, Tanzania.

Mwenyekiti wa Chadema, Mbunge wa Jimbo la Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Freeman Mbowe amesema Alhamisi Kauli ya serikali ni ya kusikitisha sana kwa sababu ni maombi gani kuhusu mgonjwa kama Tundu Lissu aliyekuwa mahututi wanataka.

Your browser doesn’t support HTML5

Mbowe ahoji dhamira ya Serikali ya Tanzania

“Hoja ya msingi ni kwamba siku tunamsafirisha Tundu Lissu kutoka Dodoma kwenda Nairobi Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alikuwa airport. Spika wa Bunge John Ndugai alikuwa airport na walikataa kuwa serikali haiwezi kuingia gharama ya matibabu kwa ajili ya Lissu. Hayo maombi wanayotaka yapelekwe, yapelekwe na nani?”

Mbowe amesema :"Lissu alikuwa anategemea maisha yake. Waziri katulazimisha tumpeleke Hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam, ambapo usalama wa maisha yake hatuna uhakika nao."

Chama hicho kiliamua kumpeleka mbunge huyo nje ya Tanzania kufanyiwa matibabu kwa kuhofia usalama wake kwa sasa, ambapo walisema iwapo watu wasiojulikana waliweza kumshambulia Tundu Lissu mchana katika eneo hilo hawawezi kuwa na uhakika juu ya usalama wake akitibiwa hapa nchini.

Your browser doesn’t support HTML5

Kauli ya serikali ya Tanzania juu ya matibabu ya Lissu

Mapema Alhamisi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu katika mkutano wake na waandishi wa habari amesema ameamua kuweka sawa mkanganyiko huo wa tuhuma kwamba serikali haitaki kuhudumia matibabu ya Tundu Lissu

Mbowe amesema kuwa waziri Ummy ametoa kauli hiyo leo baada ya kuona dunia nzima imejitolea kujaribu kumsaidia Lissu.