Cameroon na Ghana zapoteza mechi zao za ufunguzi

Mchezaji wa Ureno, Cristiano Ronaldo akishangilia baada ya kufunga bao lake la kwanza .dhidi ya Ghana katuka uwanja wa 974 Doha Qatar. November 24, 2022. REUTERS/Albert.

Michuano ya Jumatano ya kombe la Dunia inaendelea Doha Qatar ambapo nchi nyingine mbili za Afrika zilipoteza mechi zao za kwanza.

Timu ya taifa ya Cameroon Indimotible Lions ilipoteza mchezo wake dhidi ya Uswissi kwa bao 1-0 . Alikuwa ni Breel Embolo aliyepachika bao hilo la ushindi lakini alikataa kusherehekea kama ishara ya heshima kwa nchi yake ya kuzaliwa. Cameroon walijitahidi kutaka kurejea mchezoni lakini haikuwa rahisi kwao.

Na katika mechi nyingine ya kundi G siku ya Jumatano ilikuwa ni kati ya Uruguay na Korea Kusini ambapo wachezaji mahiri wa Uruguay Darwin Nunez na wakongwe Luis Suarez ambaye alitoka akaingia Edison Cavani walionyesha kwamba bado wamo.

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 0-0. Hii ilikuwa ni mechi yenye burudani na mvuto wa hali ya juu na ya kasi kubwa kwa timu zote.

Ghana yapata magoli mawili lakini wapoteza mchezo

Nao Vijana wa Black Stars ya Ghana wakiongozwa na Andre Ayew na Osman Bukari ndio walikuwa wafungaji mabao wa kwanza barani Afrika katika michuano ya mwaka huu 2022 .

Na wakati huo huo historia nyingine imeandikwa Cristiano Ronaldo anakuwa mchezaji wa kwanza katika historia kufunga katika Fainali tano za Kombe la Dunia alipopachika bao kwa njia ya mkwaju wa penati katika dakika ya 65.

Andre Ayew aliisawazishia Ghana dakika nane baadaye, lakini Joao Felix akarudisha uongozi wa Ureno na katika dakika ya 78 Rafael Leao aliongeza bao la tatu. Osman Bukari aliipatia Ghana bao la pili katika dakika ya 89.

Brazil yatamba

Wakati huo huo Brazil imeiadhibu Serbia kwa jumla ya mabao 2-0 katika mchezo mkali na wa kutumia nguvu.

Katika mchezo huo Brazil walitawala karibu mchezo wote na alikuwa ni mshambuliaji anayechezea Everton ya Uingereza Richarlison de Andre aliyepachika mabao yote mawili katika mchezo huo kupitia asisti ambazo alitoa Neymar.

Neymar majeruhi

Timu ya Serbia ilicheza kwa nguvu na kupelekea Neymar kufanyiwa faulo 9 na hatimaye kutolewa nje katika dakika ya 80 baada ya kuumia kifundo cha mguu.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari mwishoni mwa mchezo huo, daktari wa timu ya Brazil Rodrigo Lasmar alisema bado ni mapema sana kujua jinsi jeraha la Neymar lilivyo mbaya.

Mpaka sasa katika michuano hiyo kumekuwa na sare nne za bila kufungana baada ya michauno ya 2018 nchini Russia kutoa moja pekee.

Na pia rekodi ya magoli mengi kufungwa katika mchezo mmoja ambapo Spain imeicharaza Costa Rica mabao 7-0 na Uingereza kuibandika Iran mabao 6-2.

Uruguay na Korea Kusini zaanza kwa sare

Kundi G lilifunguliwa kwa mchuano mkali kati ya Uruguay, na Korea ambapo wachezaji mahiri wa Uruguay Darwin Nunez na wakongwe Luis Juarez ambaye alitoka akaingia Cavani walionyesha kwamba bado wamo.

Raundi ya kwanza imekamilika na Spain , Belgium . Brazil,Ufaransa , Ureno,Ecuador, Saudia Arabia, Uingereza, Uholanzi, Ureno wakiongoza makundi yao.

Historia yaandikwa

Historia pia imeandikwa kwa Spain kumfunga Costa Rica goli 7-0 na Saudia Arabia kuishtua dunia kwa kuifunga Argentina 2-1 na hatimaye kuongoza kundi lake.

Wakati huo huo kumewekwa historia nyingine ya marefa wa kike ambapo Salima Mukansanga ameweka rekodi ya refa mwanamke kwa mara ya kwanza katika miaka 92 ya mashindano hayo akiwa na waamuzi wenzake wa pembeni Stephanie Frappart na Yoshimi Yamashita na waamuzi wasaidizi watatu.

Mzunguko wa pili wa kombe hilo unaanza Ijumaa ambapo mmoja wa wawakilishi wa Afrika Senegal watakutana na wenyeji Qatar katika mechi ya kufa kupona wote wakihitaji ushindi ili kusonge mbele kwenye michuano hiyo.

Vile vijana wa Wales wanakumbana na Iran , Uholanzi na Ecuador na mtanange wenye upinzani mkali wa kihistoria unaongojewa kwa hamu kati ya Marekani na Uingereza.

Imetayarishwa na Sunday Shomari.