Rais wa Burundi Pierre Nkrunziza ameapisha baraza jipya la mawaziri jumanne kufuatia kuchaguliwa tena kwa muhula wa tatu wenye utata. Wanachama kutoka chama tawala cha CNDD-FDD wamepata viti 15 kati ya 20 vilivyoko vikiwemo vile vya wizara muhimu kama ulinzi, mambo ya ndani na maswala ya kimataifa.
Hatua hio haijawashangaza wapinzani wake ambao wanaamini Bw Nkurunziza alikiuka katiba kwa kuendelea kuwa ofisini. Kundi la watu maarufu kutoka Burundi wakiwemo aliekuwa makamu wa rais na spika wa bunge wamesema kuwa hawatamtambua Bw Nkurunziza kama rais baada ya kumalizika kwa kipindi cha muhula wake leo Jumatano.
Ghasia na mivutano ya kisiasa zilisababisha zaidi ya warundi 180,000 kutoroka nchini baada ya rais kutangaza nia yake ya kuwania tena urais mwezi aprili. Marekani na nchi zingine wamehimiza rais Nkurunziza kuanza mazungumzo na wapinzani wake ili kulinda udhabiti wa nchi.