Mabaraza mawili ya bunge la Russia Jumatano yameidhinisha hatua ya Rais Vladimir Putin ya kusitisha ushiriki wa Moscow katika mkataba wa kukagua silaha za nyuklia na Marekani wa mwaka wa 2010 maarufu New START.
Aliielezea hatua hiyo kama jibu la kukemea ushirika wa nchi za magharibi unaongozwa na Marekani kwa kuipa silaha Ukraine, katika juhudi za kutetea uvamizi wa mwaka mmoja wa Russia.
Putin alitangaza hatua hiyo Jumanne katika hotuba yake kuhusu hali ya taifa. Mkataba huo ambao ulikuwa unatarajiwa kumaliza muda wake mwaka wa 2026, unaweka kikomo cha usindikaji wa zana za nyuklia kwa kila nchi.
Putin alisema Russia haiwezi kukubali ukaguzi wa Marekani wa vituo vyake vya nyuklia chini ya mkataba huo, huku Washington na washirika wake wa NATO wakitoa wito wa kushindwa kwa Russia katika vita vyake nchini Ukraine.
Lakini wizara ya mambo ya nje ya Russia ilisema nchi hiyo itaheshimu vigezo vya silaha za nyuklia vilivyowekwa chini ya mkataba huo.
Rais wa Marekani Joe Biden, akizungumza mjini Warsaw Poland ambako alikutana na viongozi wa nchi za Ulaya mashiriki wanachama wa NATO zinazopakana na Russia, aliitaja hatua ya Putin ya kusitisha ushirika wa Russia katika mkataba huo wa nyuklia, kuwa “kosa kubwa”.