Bunge la Marekani lailazimisha Facebook kuthibitisha udhibiti wa siri

Mark Zuckerberg

Wabunge wa Marekani wakiwa Washington walimbana kwa maswali magumu Mkurugenzi Mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg wiki hii wakitaka aeleze jinsi kampuni yake ilivyokuwa ikitunza taarifa na siri za watumiaji wa mtandao wake.

Pia walipendekeza njia mpya ambazo wanaweza kuzitumia wao au wengine kudhibiti makampuni ya mitando ya jamii.

Mark Zuckerberg alikuwa amekabiliwa na maswali magumu ambapo wabunge wa Bunge la Marekani- Congress walitaka majibu ya maswali hayo.

Marsha Blackburn Mrepublikan amesema: “Nafikiri kile ambacho tumekifikia hapa, ni nani anaye kumiliki unapokuwa katika mitandao? Nani anamiliki haki zako unapokuwa mitandaoni?

Zuckerberg alimjibu mbunge huyo kwamba, “Naamini kuwa kila mtu anamiliki taarifa zake mwenyewe. Na hilo ndio suala la kwanza la matakwa ya huduma yetu, ukiisoma inasema hivyo.”

Congress muda mrefu lilikuwa tayari imeruhusu makampuni ya internet kufanya shughuli zake kwa usamimizi mdogo. Hisia hiyo hivi sasa imebadilika.

Mdemokrat Diana Degette amesema: “Kama ilivyokuwa tayari ni dhahiri kwa watu wengi, tumekuwa tukitegemea kampuni yenu ijisimamie yenyewe kudhibiti uendeshaji wake kwa sehemu kubwa. Hivi sasa tunatafuta njia ya kufanya kuzuia uvunjaji zaidi wa sheria.”

Lakini kampuni hizi ziko kibiashara na lengo lake ni kutengeneza kipato kwa kuweza kuonyesha kuwepo kwa watumiaji wa mitandao ambao wanalengwa na matangazo na hilo linahitaji kuwasilisha taarifa zao.

Mdemokrati Anna Eshoo ameuliza: “Je wewe (Zuckerberg) uko tayari kubadilisha mtindo wa biashara yako wenye kulinda na kuweka mbele maslahi ya mtumiaji wa mitandao?’

“Zuckerberg alijibu kwamba, hana uhakika swali hilo linamaanisha nini.”

Viongozi wa Bunge la Marekani wamekariri kutafiti kile kinachoendelea nchi za Ulaya ambako sheria mpya zinazojulikana kama Sheria za kulinda taarifa kwa jumla au GDPR ambayo itaanza mwezi ujao.

Mdemokrat Gene Green alimuuliza Zuckerberg:”Je wewe unatuhakikishia leo kwamba Facebook itatumia sheria za kulinda taarifa (GDPR) ambazo zinatumika hivi sasa Ulaya – ambazo watumiaji wa mitandao watanufaika nazo?”

Zuckerberg amejibu: “Ndiyo. Tunaamini kuwa kila mtu duniani anahaki ya kuweza kulinda taarifa zake za siri. Sisi tulikuwa na udhibiti huu kwa miaka mingi. Sheria ya GDPR inatutaka kuchukua hatua zaidi za udhibiti, na sisi tutaeneza udhibiti huo ulimwenguni.”

Wataalamu wa masuala ya siri wamesema kuwa wabunge hao wamejifunza mambo mengi katika mahojiano hayo na Zuckerberg na wako tayari kufanya mabadiliko.