Mswada wa marekebisho ya sheria ya uchaguzi wa 2022 ambao ulipokelewa Januari 20 ili kuchapishwa, haukupitishwa.
Mswada huo ulilenga kufanya uwasilishaji wa matokeo ya uchaguzi kwa njia isiyokuwa ya kielektroniki kama data ya msingi itakayotumiwa na maafisa wa uchaguzi kujumlisha matokeo ya uchaguzi.
Bunge hilo la kitaifa vile vile halikupitisha baadhi ya kanuni zinazohusiana na uchaguzi mkuu zilizowasilishwa na tume ya uchaguzi, pamoja na msajili wa vyama vya kisiasa.
Kutokana na kutozingatiwa kwa mswada huo, baadhi ya kanuni zinazohusiana na uchaguzi zitakazoathirika ni pamoja na rasimu ya marekebisho ya kanuni za uchaguzi kuhusu usajili wa wapiga kura, marekebisho ya kanuni za uchaguzi mkuu, marekebisho ya kanuni za elimu ya wapiga kura, marekebisho ya kanuni za orodha na uteuzi wa vyama vya kisiasa kuelekea uchaguzi.
Hata hivyo, bunge hilo, limepitisha mswada wa 2022 wa ugawaji wa mapato kwa serikali za majimbo , ambao bunge la Seneti linastahili kuwasilisha kwa rais Uhuru Kenyatta kuidhinishwa kisheria.
Ripoti hii imeandaliwa na mwandishi wetu wa Nairobi, Kennedy Wandera