Na BMJ Muriithi
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta Alhamisi alifanya mkutano na rais wa Nigeria Muhamadu Burari katika ikulu mjini Nairobi, ambapo wawili hao walikubaliana kwamba serikali za nchi hizo mbili zitashirikiana katika juhudi za kuuangamiza ugaidi barani Afrika.
SIKILIZA TAARIFA HIYO HAPA
Your browser doesn’t support HTML5
Wakizungumza katika mkutano huo, marais hao wawili wamesema pamoja na kushirikiana kwa maswala mengine, nchi hizo mbili pia zitatafuta uungwaji mkono na mataifa mengine ili kupambana na ugaidi ambao umeleta maafa na hasara kubwa kwa Kenya na Nigeria.
Mataifa hayo mawili yamekuwa yakilengwa na makundi ya kigaidi ya Alshabaab na Boko Haram huku wanamgambo hao wakitekeleza mauaji na uharibifu wa mali, hususan katika miaka ya hivi karibuni.
Katika taarifa yake rais Kenyatta aliongeza kuwa Kenya iko mstari wa mbele kwa kutafuta amani na usalama katika bara nzima la Afrika huku Buhari akisema kwamba mataifa yote ya Afrika yanapaswa kushirikiana kwa dhidi ya ugaidi kwa sababu uhalifu huu hauchagui."
Kenyatta alimshukuru rais Buhari kwa kuhudhuria ibada ya kumbukumbu mjini Eldoret, Kenya, siku ya Jumatano ambayo iliwaenzi wanajeshi waliouawa nchini Somalia wiki mbili zilizopita, na kusema kwamba Kenya inadhamini uungwaji mkono ilioupata kutoka kwa Nigeri kufuatia shambulio hilo la EL-ADDE.
Alisema ili kushinda vita dhidi ya ugaidi, kuna haja ya kutafuta mikakati mipya ya kupambana na mafunzo ya itikadi kali ambazo zimepelekea umwagikaji wa damu barani Afrika.
Nchi za Nigeria na Kenya zimepiga hatua nyingi katika Nyanja tofauti tofauti zikiwemo za kisiasa, kiuchumi na kijamii, licha uya kukumbwa na changamoto la ugaidi.
Aidha viongozi hao wawili wamekubaliana kuimarisha uchumi baina ya nchi hizo mbili na kusema kwamba biashara kati ya mataifa ya Afrika ni muhimu kwa kuleta umoja katika bara hilo.
Your browser doesn’t support HTML5
Lakini licha ya kupiga hatua kwenye Nyanja ya kilimo, mataifa hayo mawili yamekumbwa na changamoto ya Ufisadi ambayo imetisha kusambaratisha chomi zao. Hata hivyo marais hao wawili wamesenma watafanya kila wawezalo kuangamiza ulaji rushwa ambao umezipa taswira mbovu nchi hizo mbili.
Marais hao wawili walitarajiwa kukutana tena kwa hafla ya chakula cha jioni katika ikulu hiyo ya Nairobi. Buhari alitarajiwa kuondoka kuelekea Addis Ababa, Ethiopia siku ya Ijumaa ambako atajiunga na viongozi wengine wa nchi wanachama wa African Union akiwemo rais Kenyatta.