Kwa mujibu wa mwandishi wa VOA, Gambia inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa baada ya Rais Jammeh kukataa kukubali ushindi wa Adama Barrow katika uchaguzi wa Disemba 1.
Wawakilishi wa baraza kuu la bunge wamejadili hoja ya ushauri Alhamisi kama ni sehemu ya juhudi za mazungumzo ya amani yanayoendelea katika kukabidhiana madaraka katika taifa dogo la Afrika Magharibi.
Mwakilishi wa baraza hilo, Mohammed Zorro alianzisha hoja hiyo ya pendekezo la kutoa fursa ya hifadhi ya kisiasa, akisema kuwa iko katika maslahi makubwa ya Nigeria kusaidia kuhakikisha kuna amani nchini Gambia.
“Ni desturi ya kawaida katika viwango vya kidiplomasia kila mahali kuwapokea wakimbizi, kama vile viongozi walioondolewa madarakani au marais ambao wameshindwa uchaguzi au waliokimbia matatizo ya kisiasa. Na hii ndio sababu hivi sasa tunaona huu ni mchango wa bunge, kumpa nguvu rais wa Nigeria, Jenerali Muhammadu Buhari kufanya hivyo.
Zorro ameongeza kuwa pia kuna sababu nyingine, akisema kuwa, “Nigeria ina maslahi ya kimkakati; sisi tuna taasisi za fedha ambazo zinafanya biashara nchini Gambia. Tunayo mashirika ya ndege yakitoa huduma kutoka Nigeria kwenda Gambia. Tumewekeza mno katika kutoa mafunzo kwa viongozi wa Gambia katika nyanja mbalimbali.”
Lakini kuna wanaofikiria kuwa Jammeh ananang’ania katika madaraka ili asiweze kufunguliwa mashtaka ya makosa ya jinai. Utawala wake wa miaka 22 ulikuwa umegubikwa na madai ya uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu.
Pia pendekezo hili la kumpa hifadhi linalotokea Nigeria limekusudia kumshinikiza Jammeh aachie madaraka, amesema mwanaharakati Echezona Asuzu anayeishi Abuja.