Boti lenye zaidi ya watu 100 lapata ajali ziwa Kivu, DRC

Ziwa Kivu, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, watu watatu wamefariki katika ajali ya boti katika ziwa Kivu, mashariki mwa nchi hiyo.

Shughuli ya kutafuta watu wengine 40 inaendelea, zaidi ya 50 wameokolewa.

Walionusurika wameambia sauti ya Amerika kwamba boti lilikuwa limebeba zaidi ya watu 100 pamoja na mizigo na lilipinduka kufuatia dhoruba kali.

Maafisa wamesema kwamba ajali hiyo imesababishwa na hali mbaya ya hewa.

Boti hilo lilikuwa limebeba watu na mizigo kuzidi kiasi.

Maafisa pia wamesema kwamba boti lililohusika katika ajali liliundwa kwa ajili ya kubeba mizigo na wala sio binadamu.

Ajali za boti hutokea kila mara nchini Jamhuri ya kidmokrasia ya Congo na kusababisha vifo vya watu kadhaa kila mwaka.

Imetayarishwa na Austere Malivika, VOA, Goma