Afisa wa serikali ya Kenya amesema kuwa wafanyakazi wa misaada wanne Kenya wamepoteza maisha baada ya gari yao kukanyaga bomu karibu na kambi ya wakimbizi ya Dadaab katika kaunti iliyoko mashariki mwa Garissa.
Mohamud Saleh, mratibu wa mkoa wa kaskazini mashariki, amesema Jumanne gari hilo ni mali ya shirika la African Development Solutions. Amesema inadhaniwa kuwa bomu hilo lilikuwa limetegeshwa na kikundi cha siasa kali ya al-Shabab ambacho kiko nchi ya jirani ya Somalia.
Sio chini ya watu 34 wamepoteza maisha mpaka sasa wakiwemo maafisa wa polisi 20, katika milipuko Kenya katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.
Wachambuzi wanasema ni mabadiliko ya mkakati wa al-Shabab, ambayo imekuwa ikifanya mashambulizi ndani ya Kenya tangu 2011. Kikundi hicho chenye siasa kali kimeeleza shambulio hilo ni kulipiza kisasi juu ya Kenya kupeleka vikosi vyake kupambana na wapiganaji hao ndani ya Somalia.