Bobi Wine amtaka Museveni kuwajibika

Waandamanaji nchini Uingereza wakipinga utawala wa Rais Yoweri Museveni, Agosti 23, 2018.

Mbunge maarufu nchini Uganda, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, amemtaka Rais Yoweri Museveni kuwajibika kwa wananchi anao waongoza na kukomesha dhulma na mauaji yanayo "fanywa" na maafisa wa usalama dhidi ya raia.

Bobi Wine ametoa wito huo wa moja kwa moja kwa Rais Museveni, wakati serikali ya Marekani ikitaka mashataka ya uhaini dhidi ya Bobi Wine na wenzake 32 kufutiliwa mbali.

Tamko la serikali ya Marekani

Serikali ya Marekani inaitaka serikali ya Uganda kufutilia mbali mashtaka ya uhaini dhidi ya Mbunge Bobi Wine na wenzake 32, ikisema kwamba mashtaka hayo ni ya kupangwa.

Baraza la Wawakilishi Marekani, limemwandikia barua balozi wa Uganda nchini Marekani, Mull Katende likitaka uchunguzi wa kina na usioegemea upande wowote ufanyike, kubaini aliyekosa katika vurugu za Arua, zilizo pelekea dereva wa Bobi Wine, kuuwawa kwa kupigwa risasi.

Baraza hilo vile vile limeeleza kusikitishwa na vitendo vya maafisa wa polisi vya kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia wa Uganda hasa wafuasi wa upinzani.

Katika ujumbe wa moja kwa moja kwa Rais Yoweri Museveni, kupitia kikao na vyombo vya habari nyumbani kwake, nje kidogo ya jiji la Kampala, Bobi Wine anamtaka Museveni kubadili msimamo wake wa kile amekitaja kama dhulma dhidi ya wabunge, na raia walio na mawazo tofauti jinsi taifa la Uganda linastahili kuongozwa.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa Bobi Wine anataka Rais Museveni kuzungumzia hisia zake kuhusu watu wanaoendelea kuuwawa na maafisa wa usalama kote nchini kwa sababu wanapinga utawala wake.

Madai ya raia kudhulumiwa

"Nataka kujua jinsi unavyohisi unavyowadhulumu watu wako kiasi hiki Rais Museveni. Unahisi vipi unapoendelea kukanyaga shingo za watu wako kila mara wakati wamelala chini hoi? Mara nyingi umesema kwamba wewe ni babu yetu lakini vitu unavyo fanya sio vitu babu huwafanyia wajukuu zake. Babu ana upendo na moyo wa huruma, lakini wewe, umejaa dhuluma na manyanyaso," amehoji Bobi Wine.

Bobi wine vile vile amedai kwamba kuna juhudi za maafisa serikalini kusajili chama kinachoitwa "people’s power" yaani nguvu za watu , na baadaye kutangaza kuwa kundi la waasi ili kuwakamata wabunge na raia wanaojihusisha nacho, dhamira kuu ikiwa kumaliza nguvu harakati za kisiasa za wapinzani.

Vile vile, anawataka maafisa wa usalama kuwajibika na kujua kwamba wana wajibu mkubwa wa kulinda raia na mali yao na wala sio kuwaua.

Madai dhidi ya vyombo vya usalama

"Na kwa ndugu na dada zetu wanaovaa sare za usalama, nataka kuwakumbusha kwamba nyinyi ni raia wa Uganda kabla na baada ya kuwa afisa wa polisi au wa jeshi. Msitumie nafasi na bahati mliopata kuwa maafisa wa usalama kuwadhulumu raia wenzenu kwa sababu mnataka kutetea utawala unao watesa raia," amesema mwanasiasa huyo.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, VOA, Washington DC.