Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Lammy, Jumanne amekuwa mwenyeji wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, mjini London, kujadili masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na vita vya Gaza, na Ukraine.
Maafisa wa Uingereza na Marekani pia wanaangazia uhusiano wa mataifa hayo mawili pamoja na masuala yanayohusiana na eneo la Indo Pacific.
Lammy katika taarifa yake kabla ya kikao chake na Blinken alisema kuwa, “ Katika ulimwengu hatari na usio na usalama, ni muhimu zaidi kuwa na ushirikiano wa kimataifa.”
Blinken baadaye anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer, ambaye chama chake kilirejea madarakani hapo Julai, kwa mara ya kwanza baada ya miaka 14. Starmer pia anatarajiwa kukutana na rais wa Marekani Joe Biden, Ijumaa, hapa mjini Washington.