Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken ameanza ziara yake ya mataifa matatu katika bara la Afrika kwa onyo kwamba mambo kadhaa yamesababisha kuporomoka kwa demokrasia kote duniani.
Akizungumza mbele ya kundi la wanaharakati wa haki za binadamu leo Jumatano mjini Nairobi huko Kenya, Blinken alisema hata demokrasia iliyochangamka kama Kenya imekuwa hatarini zaidi kwa taarifa zisizo sahihi, ufisadi, ghasia za kisiasa, na manyanyaso kwa wapiga kura.
Marekani haina kinga kutokana na changamoto hii, Blinken alisema akikumbushia shambulizi la januari 6 lililofanywa na wafuasi wa rais wa wakati huo Donald Trump dhidi ya bunge la Marekani katika jaribio la kuwalazimisha wabunge kufutilia mbali ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi mkuu wa rais wa Novemba mwaka 2020. Tumeona jinsi demokrasia yetu tete inavyoweza kuingiliwa.
Mwanadiplomasia huyo wa cheo cha juu Marekani aliwaambia washiriki kwamba alitaka kusikia mitazamo yao kuhusu changamoto za kidemokrasia, na mawazo yao juu ya kutatua hali hiyo, pamoja na jinsi gani Marekani inaweza kusaidia juhudi hizi.