Blinken atembelea Misri na Qatar kuhusu Gaza

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken, ametembelea mataifa wapatanishi Misri na Qatar, Jumanne kutafuta makubaliano ya kusitisha mapigano ya vita vya Gaza.

Amesema ni wakati muhimu, alipokuwa akimalizia ziara yake ya tisa mashariki ya kati.

Lakini Hamas na Israel ziliashiria kuwa haziafiki vipengele vya mapendekezo yanayoungwa mkono na Marekani, na makubaliano yalionekana kuwa magumu kama hapo awali.

Katika taarifa yake mpya, Hamas imesema pendekezo la karibuni linageuza kile ilichokubali hapo awali na kuishutumu Marekani kwa kuafiki kile ilichokiita masharti mapya kutoka kwa Israel.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amewaambia ndugu wa mateka waliopo Gaza kwamba lengo kuu ni kuhifadhi mali zao za kimkakati za usalama katika kukabiliana na shinikizo kubwa kutoka ndani na nje ya nchi.