Blinken ametangaza dola bilioni 2 za kufadhili juhudi za kijeshi za Ukraine

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken akizungumza na waandishi wa habari mjini Kyiv. May 15, 2024.

Tangazo hilo linakuja wakati wanajeshi wa Ukraine wakirejea kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kufuatia mapigano

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ametangaza Jumatano dola bilioni 2 kufadhili juhudi za kijeshi za Ukraine wakati akihitimisha ziara yake ya siku mbili huko Kyiv.

Tangazo hilo linakuja wakati wanajeshi wa Ukraine wakirejea katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo kufuatia mapigano makali na vikosi vya Russia. Russia siku ya Jumatano ilisema vikosi vyake viliyateka makazi mengine mawili katika mkoa wa Kharkiv, ambako vikosi vya Russia vimekuwa vikizidisha mashambulizi yao.

Jeshi la Russia pia lilishambulia Shevchenkivsky, wilaya ya kati ya Kharkiv, kulingana na gavana wa mkoa Oleh Syniehubov, ambaye aliandika kwenye mtandao wa Telegram kwamba shambulio hilo liliwajeruhi watu wawili na kuharibu jengo la ghorofa tano.

Mashambulizi hayo yalimfanya rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy kuahirisha ziara zijazo za nje ya nchi.