Binti ya Dos Santos apinga kuzikwa kwake Angola

Mtoto wa kike wa Dos Santos ,Tchize dos Santos.

Mtoto wa kike wa  aliyekuwa rais wa Angola Eduardo dos Santos Alhamisi amewasilisha rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama ya Spain   kwamba mwili wa baba yake ukabidhiwe kwa mjane wake Ana Paula ili urejeshwe  Angola kwa mazishi.

Dos Santos aliyetawala taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta kuanzia 1979 hadi 2017 alifariki Julai 8 mjini Barcelona, Spain, akiwa na umri wa miaka 79, kufuatia matatizo ya moyo. Tangu wakati huo suala la wapi na lini atazikwa limezua mivutano kati ya serikali ya Angola na mjane wake Ana Paula pamoja na baadhi ya watoto wake.

Kwa mujibu wa shirika la habari AFP. Binti wa Dos Santos, Tchize dos Santos mwenye umri wa miaka 44 amepinga uamuzi wa mahakama akisema kwamba baba yake alitamani kuzikwa Barcelona, alikokuwa akiishi tangu kuondoka madarakani 2017.

Ameongeza kwamba kuzikwa kwa baba yake nchini Angola kutatumika kuonyesha umaarufu wa serikali ya rais Joao Lourenco kuelekea uchaguzi mkuu unaofanyika Agosti 24. Rufaa ya Tchize pia inadai kwamba Ana Paula alikuwa ametengana na Dos Santos tangu 2017, na kwa hivyo hawezi kudai kuwa mke wake.