Bilionea wa China afungwa miaka 13 na kampuni yake kupigwa faini

Picha ya Maktaba: Bilionea wa China, akiwa nje ya kituo cha kimataifa cha fedha, Hong Kong Desemba 2013.

Mahakama ya Shanghai, Ijumaa imemuhukumu bilionea wa Kichina mwenye uraia pia wa Canada, Xiao Jianhua, ambaye hajaonekana hadharani toka 2017, kifungo cha miaka 13 gerezani na kupigwa faini kampuni yake ya Tomorrow Holdings dola bilioni 8.1 ikiwa ni rekodi kwa China.

Bilionea Xiao na kampuni ya Tomorrow Holdings, zilishutumiwa kufanya mihamala kinyume cha sheria katika hifadhi za fedha za umma, kuvunja uaminifu, na matumizi ya fedha kinyume cha sheria pamoja na rushwa imesema mahakama ya Shanghai.

Imeongeza kusema hukumu hiyo imekuwa hivyo kwa sababu pande zote zilikiri kufanya makosa hayo na kutoa ushirikiano katika kuokoa fedha zilizo chukuliwa kinyume cha sheria na kurejeshwa kwake.

Xiao ambaye amezaliwa China na kufahamika kuwa na uhusiano na viongozi wa juu wa chama cha Kikomunisti cha China, kwa mara ya mwisho alionekana akiwa katika kiti cha magurudumu katika hoteli ya kifahari ya Hong Kong katika saa za mapema akiwa amefunika kichwa chake kimesema chanzo cha karibu na shirika la habari la Reuters.