Biden na Trump kukutana White House Jumatano

  • VOA News

Rais wa Marekani Joe Biden, na Rais mteule Donald Trump.

Rais wa Marekani Joe Biden atazungumzia masuala muhimu, ya sera za ndani na za kigeni, yanayohitaji kupewa kipaumbele, wakati wa mkutano wake na Rais mteule Donald Trump Jumatano.

Biden pia huenda akachukua nafasi hiyo kumsishi kuendelea kusaidia Ukraine baada ya kuchukua madaraka, mshauri wa usalama wa kitaifa Jake Sullivan amesema Jumapili. Trump, wa chama cha Republikan, ataapishwa kuwa rais hapo Januari 20, baada ya kumshinda mgombea wa chama cha Demokratik, naibu wa Rais Kamala Harris.

Kwenye mahojiano ya Jumapili na televisheni ya CBS, kipindi cha Face the Nation, Sullivan alisema kuwa ujumbe mkuu wa Biden kwa Trump utakuwa kukabidhiana madaraka kwa njia ya amani, wakati pia wakishauriana kuhusu kinachoendelea Ulaya, Asia na Mashariki ya Kati. Ingawa hakueleza kwa kina kuhusu mazungumzo ya viongozi hao, alisema kuwa suala la vita vya Russia na Ukraine ni lazima liwepo kwenye ajenda yao.

Trump wakati wa kampeni aliahidi kumaliza vita hivyo, ingawa haukeleza ni kwa njia gani. Sullivan pia alisema kuwa Biden ana nafasi katika siku 70 alizobakisha madarakani, ya kushawishi bunge pamoja na utawala ujao kuhusu umuhimu wa kuendelea kuunga mkono Ukraine, kwa kuwa kutofanya hivyo kunahatarisha Ulaya.