Biden kukutana na mfalme wa Jordan mjini Washington

  • VOA News

Mfalme wa Jordan Abdullah bin Al-Hussein.

Rais wa Marekani Joe Biden,  Jumatatu atakuwa na mazungumzo na  Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan, kwenye White House, mjini Washington DC, juu ya suala la kuachiliwa mateka waliopo Gaza, pamoja na kuongezeka kwa wasi wasi kutokana na operesheni za kijeshi za Israel kwenye mji wa bandari wa Rafah.

Hicho ndicho kikao cha kwanza cha washirika hao tangu kuuwawa kwa wanajeshi watatu wa Marekani mwezi uliopita kwenye shambulizi la droni katika kituo kimoja cha kijeshi cha Marekani nchini Jordan.

Biden alilaumu wanamgambo wa ki-Houthi wanaoungwa mkono na Iran kwa shambulio hilo, likiwa la kwanza dhidi ya Marekani nchini humo, baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi kutoka kwenye makundi kama hayo, dhidi ya wanajeshi wa Marekani, kote Mashariki ya Kati, tangu kuzuka kwa vita vya Israel na Hamas.

Mkutano wao unafanyika wakati Biden na washauri wake wakijitahidi kuitisha sitisho lingine la mapigano kati ya Israel na Hamas, ili kuruhusu kupelekwa kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza, pamoja na kuachiliwa kwa mateka wa Israel wanaoendelea kushikiliwa.