Biden kukagua mradi mkubwa wa reli wakati wa ziara ya Angola Desemba

  • VOA News

Bandari ya Lobito ya Angola

Wakati wa ziara ya Rais wa Marekani Joe Biden mapema mwezi ujao nchini Angola, ataangazia mradi wake mkubwa wa kimiundomsingi, unaolenga kuunganisha usafirishaji wa bidhaa barani Afrika.

Mradi huo wa reli kwa jina Lobito Corridor, ni kipaumbele cha mkakati wake wa kukabiliana na ushawishi wa China kwenye maendeleo ya kimataifa. Lobito Corridor ni mradi unaogharimu dola bilioni 5 kwenye sekta kadhaa kwa lengo la kukarabati na kuongeza njia ya reli ya Benguela yenye urefu wa kilomita 1,300.

Reli hiyo itaunganisha bandari ya Angola ambayo imekuwepo kwa miaka 120 ya Lobito katika bahari ya Atlantic, hadi kweye Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na kisha baadaye ifike Zambia. Ufadhili mkubwa wa mradi huo uliotangazwa Septemba 2023 unatoka kwenye kundi la Ushirikiano wa Kimataifa wa Miundomsingi na Uwekezaji, PGI, lililoanzishwa na Biden 2022 akishirikisha mataifa ya G7.

Mradi huo utakapokamilika, utakuwa muhimu katika kusafirisha madini kwa Marekani na washirika wake yakiwemo shaba na cobalt, ambayo ni muhimu kwenye utengenezaji wa magari ya kutumia umeme. Kulingana na ripoti iliotolewa na Baraza la Congress la Marekani, asilimia 80 ya migodi ya shaba ya DRC inamilikiwa na China.