Biden atangaza njia mpya za kuwasaidia wamarekani kupata chanjo dhidi ya Corona

Mfano wa chanjo dhidi ya virusi vya Corona

Rais Biden alitoa wito kwa kampuni zinazoendesha usafiri wa Lyft na Uber kutoa usafiri wa bure kwenda na kutoka kwenye maeneo yanayotoa chanjo kwa mtu yeyote anayepata chanjo ifikapo Julai nne

Rais wa Marekani Joe Biden, Jumanne ametangaza njia mpya za kuwasaidia wamarekani wengi kupata chanjo dhidi ya janga la virusi vya Corona.

White House ilisema kwamba wakati Biden alipokutana na kundi la magavana sita wa Marekani kutoka pande mbili, alielezea mipango yake kwa kampuni zinazoendesha usafiri wa Lyft na Uber, kutoa usafiri wa bure kwenda na kutoka kwenye maeneo yanayotoa chanjo kwa mtu yeyote anayepata chanjo ifikapo Julai nne.

Tarehe hiyo ni maadhimisho ya kila mwaka ya siku ya uhuru wa Marekani ambapo Rais Biden ameweka lengo kwa asilimia 70 ya wamarekani watu wazima, wawe wamepatiwa angalau dozi moja ya chanjo.

Takwimu hivi sasa zipo kwenye kiwango cha asilimia 58. Biden pia alitangaza baadhi ya vyuo vikubwa vya jamii nchini Marekani, vitatumika kama maeneo ya kutolea chanjo kwa wanafunzi, wafanyakazi na jamii kwenye maeneo hayo kwa mwezi Mei na June.