Biden asema kuondoka kwa Assad ni nafasi ya wa -Syria kukomboa nchi yao

  • VOA News

Rais wa Marekani Joe Biden.

Rais wa Marekani Joe Biden Jumapili amesema kuwa kuanguka ghafla kwa serikali ya Syria ya Bashar al Assad ni “kitendo cha msingi cha  haki,” lakini ni wakati wa kutokuwa na uhakika kwa Mashariki ya Kati.

Akizungumza akiwa kwenye White House, Biden alisema kuanguka kwa utawala huo wa kiimla wa miongo kadhaa chini ya familia ya Assad ni fursa muhimu kwa kizazi cha watu wa Syria kuamua hatima yao.

Biden amesema kuwa hatua za Marekani na washirika wake ndani ya miaka miwili iliyopita zilidhoofisha washirika wa Syria wakiwemo Russia, Iran na kundi la Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran, kiasi kwamba kwa mara ya kwanza walishindwa kuilinda serikali ya Assad. “Mwelekeo wetu umebadili madaraka katika Mashariki ya Kati,” Biden alisema baada ya kukutana na washauri wa taifa wa usalama huko White House.

Rais mteule wa Marekani Donald Trump Jumapili kwa upande wake alisema kuwa Assad ameikimbia nchi, ambayo familia yake iliitawala kwa miongo kadhaa, kwasababu mshirika wake Vladimir Putin, Rais wa Russia, “hakuwa tena na haja ya kumlinda.” Matamshi ya Trump kwenye mitandao ya kijamii yamekuja siku moja baada ya kuelezea kuhusu uwezekano wa Marekani wa kuingilia kijeshi nchini Syria, ili kuwasaidia waasi wakati wakisonga mbele kumuondoa Assad. “HIVI SI VITA VYETU,”Trump alisema.