Biden anasema ana matumaini ya kuona sitisho la mapigano huko Gaza

Rais wa Marekani Joe Biden

Makubaliano yatajumuisha kuachiliwa huru mateka wanaoshikiliwa na pande zote za Israel na Hamas

Rais wa Marekani Joe Biden amesema ana matumai ya kuona sitisho jipya la mapigano Gaza kufikia mapema wiki ijayo, wakati wajumbe kutoka nchi kadhaa wakifanya kazi kushauriana kusitisha mapigano kwa mara ya kwanza tangu mwishoni mwa mwezi Novemba.

Mshauri wangu wa usalama wa taifa ananiambia tunakaribia, Biden aliwaambia waandishi wa habari mjini New York. Tulikuwa karibu. Bado bado hatujamaliza. Matumaini yangu kufikia Jumatatu ijayo tutakuwa na sitisho la mapigano. Wasuluhishi wamekuwa wakifanyia kazi kuelekea makubaliano ambayo yatasitisha mapigano kwa wiki sita.

Makubaliano hayo yatajumuisha kuachiliwa huru kwa mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas huko Gaza, pamoja na kuachiliwa huru kwa wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel.

Mamia ya malori ya misaada ya kibinadamu yataingia Gaza kila siku, pia yatakuwa sehemu ya makubaliano hayo.