Mpinzani mkuu wa serikali ya Uganda, Dr. Kiiza Besigye amesema chama chake kitatumia mbinu zote zisizo za kivita kuleta mabadiliko nchini Uganda.
“Ni lazima tuchukue hatua zisizo na fujo au ghasia kudhoofisha nguvu ya udikteta,” alisema Jumatatu.
Mwandishi wa VOA Kennes Bwire aliyoko Uganda anasema Besigye amesisitiza kuwa wakulima wakikataa kupeleka chakula sokoni, hakuna namna utawala unaweza kukabiliana na hilo, kwani hawa wote wanaotumia bunduki hawataweza kuzibeba kwa sababu ya njaa hatua ambayo itafanikisha malengo yetu.
Your browser doesn’t support HTML5
Akijitambulisha kama rais wa watu wengi walioko Uganda, Besigye amebainisha kuwa ameunda makundi vijijini yanayoendelea kupanuka na kujikita tayari kuchukua hatua aliyoiita; kurejesha madaraka kwa raia.
Aliongeza kusema kwamba yote anayofanya siyo ya siri wala hayapelekei uvunjaji wa sheria.
Alisema yuko huru kuwaeleza waandishi wa habari hatua za chama chake cha Forum for Democratic Change zenye lengo la kuongoza Uganda kwa namna ambayo waganda wanavyotaka na hakuna kitakacho mzuia.
“Utakapotakiwa kuchukua hatua uwe uko tayari,” alisema kiongozi huyo.
Ameiita hatua hii siyo ya kivita katika juhudi za upinzani kufanikisha malengo yake, akisema kati ya hatua hizo ni migomo ya wafanyakazi kufika kazini, wafanya biashara kufunga maduka yao na wateja kukataa kununua baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa na kuuzwa na wale walioko madarakani.
Aliongeza kuwa imefika wakati kwa Chama chake kuchukua hatua za kuwarai wafuasi wake kutekeleza migomo hiyo.
“Tutaweza kuwashinda hata utawala uliokuwa na nguvu za kupindukia ikiwa tutafanya hivyo,” alisema Besigye.
Kwa mujibu wa mwandishi wa VOA Besigye hata hivyo amesema chama chake kipo tayari kwa mazungumzo iwapo yataongozwa na mtu asiyegemea upande wowote kisiasa na kuwa yafanyike baada ya ukaguzi wa kimataifa wa kura za mwaka 2016.
Lakini katika ujumbe wa mwaka mpya, rais Yoweri Museveni amesema yuko tayari kukabiliana na mtu yeyote atakayeleta vurugu katika utawala wake.
Ametoa mfano jinsi anavyo kabiliana na watu wanaopanga vita, akiwa na maana ya mauaji ya watu yaliyotekelezwa na serikali dhidi ya Ufalme wa Rwenzururu Desemba mwaka jana.