Afisa mmoja kutoka chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change-FDC nchini Uganda, alisema Ijumaa kuwa kiongozi wa chama hicho, Kizza Besigye, ambaye ameshindwa uchaguzi mara tatu akiwania kupata nafasi ya kiti cha rais nchini humo dhidi ya Rais Yoweri Museveni, anatarajia kujiuzulu.
Katibu Mkuu wa chama cha FDC, Alice Alaso aliliambia shirika la habari la AFP “Imethibitishwa kwamba atajiuzulu. Taarifa imewasilishwa na kukubaliwa na kamati ya chama kitaifa”. Alaso alisema kwamba tarehe kamili ya kuacha kazi Besigye ilikuwa bado haijapangwa, lakini haitachukua muda mrefu”.
“Tunafanya kazi juu ya mipango ya muda ya kumsaidia kukabidhi madaraka kwa atakayemrithi,” alisema Alaso, akielezea kwamba kujiuzulu kwa Besigye hakutamzuia kuwania tena nafasi ya kiti cha rais katika uchaguzi wa mwaka 2016.
Besigye, daktari wa zamani wa Museveni anaonekana kuwa mwanasiasa pekee wa upinzani ambaye anaweza kutoa changamoto katika utawala wa miaka 25 wa Rais Yoweri Museveni.
Kiongozi huyo wa upinzani amekamatwa mara kwa mara na kufikishwa mahakamani nchini humo tangu yalipoanzishwa maandamano mwaka jana dhidi ya ongezeko la bei za bidhaa.
Besigye alizaliwa April 22 mwaka 1956 katika eneo la Kasangati nchini Uganda. Alipata shahada ya udaktari katika chuo kikuu cha Makerere mjini Kampala, Uganda. Alipata mafunzo ya kijeshi na mwaka 1980-1986 alijiunga na kundi la National Resistance Army-NRA, waasi wa msituni dhidi ya serikali ya Rais Milton Obote. Aliwajibika kwenye kundi hilo kwa afya za wanajeshi hao wa msituni na alihusika hasa kwa mwenyekiti, Yoweri Museveni.
Uongozi wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change nchini Uganda umethibitisha taarifa ya kujiuzulu Bessigye